🇹🇿 Kwa lugha nyepesi ya Kiswahili fasaha, Kiunguja, Ibrahim Mohammed Hussein, anasimuliya kwa uwazi na ujasiri mkubwa, yale yaliyomsibu baada ya kuuwawa Rais wa Kwanza wa iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume. Tukio hilo la siku ya Ijumaa, tarehe 7 Aprili 1972, liliigubika nchi katika giza zito na kuzusha hamkani ya nguo chanika. Maisha Visiwani yakawa sio shwari tena. Kamatakamata ikawa ndio kilio kilichosikisika mitaani. Mwandishi wa kitabu hichi nae pia akanaswa ndani ya mtego wa panya, ulioingiza waliokuwemo na wasiokuwemo. Kilichomponza ni u-Ahlil Barza wake na Baraza ya Majestic, iliyokuwa katikati ya Mji Mkuu wa Zanzibar, aliyokuwa akijipumzisha kwa soga na maskhara na ahlil barza wenzake. Mithili ya chozi jichoni, tone la wino wa kalamu ya mwandishi, linasononeka kwa kuyanukuu madhila yaliyomkumba na kupelekea kunyang’anywa utu wake na hadhi yake kama binadamu. Mwili wake, kama wa madhulumu wenzake, uligeuzwa kama ngoma kucharazwa kwa vyuma na magongo ya mipera na milimau. Maisha yakawa hayana stara. Utupu wake kama ule wa wenzake haukutafautishwa na wa mnyama. Wote walilazimishwa kufanya haja zote mbele ya hadhara wakati wengine wakisubiri zamu zao.
Ladha na utamu wa lugha aliyoitumia mwandishi kuielezea kadhia yake, yenye kusisimua na kuhuzunisha sana, inamfanya msomaji kuwa na raghba ya kukisoma kitabu bila ya kusita. Kila ukurasa unamsogeza karibu na pazia zito lililogubikwa, kwa miaka nenda miaka rudi, na mengi nyuma yake yasiyoweza kutarajiwa na hata kufikirika katika mazingira ya maisha na malezi ya Kizanzibari. Mwenye kuifahamu Zanzibar iliyokuwa imejengeka katika misingi ya dini ya Kiislamu, Imani, Utu na Ubinaadamu atapigwa na bumbuwazi kuyasoma yaliyokuwa yakijiri nyuma ya lango kuu la Jela ya Kiinua Miguu, hususan upande ule maarufu wa Kwa Bamkwe, uliokuwa kama Milki moja ya mungu Mtu, ambae wafuasi wake nao wakijiona kama ndio kina Munkar na Nakir wa humo ndani. Majahil waliotakabar hadi kufikia mpaka kiongozi wao mkuu, Mandera, kuthubutu kuwaambia madhulumu wake kwamba « huko nje Mungu ndiye mwenye kutowa rizki » lakini kule ndani, kwenye milki yake, ni « yeye mwenye kutowa rizki ». Ndani ya Jumba la Maafa, mwandishi anampitisha msomaji wake katika kuta na vichochoro vya mateso yaliyokithiri na watesaji waliofurutu ada kwa ukatili wao, mithili ya vikosi thakili vilivyokuwa vikitajika duniani, Gestapo (Ujerumani ya Aldof Hitler) na Tonton Macoutes (Haiti ya Duvallier). Kuta zilizosheheni sauti za vilio vya idhilali na mateso. Kuta zilizoyaona maafa mengi ya madhulumu waliotolewa roho zao mbichi au kutiwa vilema vya maisha vya kimwili na kiakili kwa kulazimishwa kukiri makosa wasiyoyajuwa.
Mwandishi kama madhulumu wenzake wengine hakuwahi kupata uaidhi, ushauri wa kisaikolojia, baada ya kutoka jela. Jitihada zake za kuyaeleza yaliyomsibu na kumkwaza rohoni kupitia kitabu hichi, ni hatua moja kubwa muhimu katika harakati zake za kuitibu nafsi yake.
🇫🇷 Ibrahim Mohammed Hussein fut arrêté le 11 avril 1972, dans le sillage de l'assassinat du Président Karume à Zanzibar, à la suite d’accusations infondées le liant à cet attentat comme "traître à la révolution". Initialement condamné à mort, il passa plus de six années en prison, où il endura des tortures inhumaines, dans la partie de la prison de Kiinua Miguu célèbrement connue de "Kwa Bamkwe", qu'il qualifie "d'abattoir". À la différence de l'écrivain swahili Adam Shafi, qui dans son ouvrage "Haini" a choisi une approche allégorique et l'usage de pseudonymes pour relater les sévices qu'il a subis et les violations des droits humains à Zanzibar, Hussein opte pour une narration directe et sans fard. Ce livre en swahili constitue une étape cruciale pour la vérité et la réconciliation sur l'île de Zanzibar après la révolution et représente, au moins sur le plan thérapeutique, une avancée vers la reconstruction des victimes de la vague d'arrestations arbitraires de l'époque. C'est aussi un témoignage précieux et une occasion de réflexion sur les violations des droits humains dans les prisons et les moyens à mettre en place pour les prévenir.
- Date de publication
- 24 juillet, 2024
- Langue
- Swahili
- ISBN
- 9781445248967
- Copyright
- All Rights Reserved - Standard Copyright License
- Contributeurs
- Par (auteur): Ibrahim Mohammed Hussein, Preface par: Ahmed Rajab, Edité par: Mohamed A. Saleh
- Pages
- 202
- Dimensions
- A5 (5.83 x 8.27 in / 148 x 210 mm)
Baraza ya Majestic na Machinjioni kwa Bamkwe
Kwa lugha nyepesi ya Kiswahili fasaha, Kiunguja, Ibrahim Mohammed Hussein, anasimuliya kwa uwazi na ujasiri mkubwa, yale yaliyomsibu baada ya kuuwawa Rais wa Kwanza wa iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa ...
Buy the Paperback, WorldWide
Baraza ya Majestic na Machinjioni kwa Bamkwe
(swa) Kwa lugha nyepesi ya Kiswahili fasaha, Kiunguja, Ibrahim Mohammed Hussein, anasimuliya kwa uwazi na ujasiri mkubwa, yale yaliyomsibu baada ya kuuwawa Rais wa Kwanza wa iliyokuwa Jamhuri ya ...
https://books.google.fr/books/about?id=bckVEQAAQBAJ&redir_esc=y
free previex (extracts only) in Google Books
Pitio la Kitabu: Baraza ya Majestic na Machinjioni Kwa Bamkwe
Source : http:// https://www.jamiiforums.com/threads/pitio-la-kitabu-baraza-ya-majestic-na-machinjioni-kwa-bamkwe.2246726/ (tumesoma tarehe 17 Agosti 2024)
Hiki ni kitabu cha nne ambacho nimekifanyia patio katika vitabu ambavyo vinaeleza mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. Kitabu cha kwanza kilikuwa kitabu cha Dr. Harith Ghassany ambacho nilishiriki katika utafiti wake kama msaidizi wa Dr. Ghassany: ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,’’ (2010); kitabu cha pili ni nilichofanya patio ni alichoandika Muhammad Al – Marhuby: ‘’His Life and Legacy My Father Amor Ali Ameir,’’ (2016); kitabu cha tatu ni cha Hashil Seif: ‘’Mimi Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar,’’ (2018); kitabu hiki nilialikwa hapa ZIRPP kukiwasilisha na ndiyo mara yangu ya kwanza kuzungumza katika ukumbi huu; kitabu cha nne cha Zuhura Yunus: ‘’Biubwa Amour Zahor Mwanamke Mwanamapinduzi,’’ (2021), kitabu cha tano ni cha ‘’Theoretician,’’ Khamis Abdallah Ameir: ‘’Maisha Yangu,’’ (Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi: Khaini su Mhanga wa Mapinduzi?) (2022) hiki ni kitabu change cha pili kukihudhurisha hapa ZIRPP, na hiki kitabu cha sita cha Ibrahim Hussein, ‘’Baraza ya Majestic na Machinjioni kwa Bwamkwe.’’ (2024) ni kitabu change cha tatu kualikwa kukuzingumza ZIRPP.
Kuna vitabu vingine nimevieleza ingawa siwezi kusema nilifanya patio mfano. Katika vitabu hivi ni kitabu cha Aman Thani: ‘’Ukweli ni Huu’’ (1995); Ali Muhsin Barwani: ‘’Conflict and Harmony in Zanzibar,’’ (1997), ambacho kilifanyiwa tafisiri, ‘’Kujenga na Kubomolewa Zanzibar,’’ kitabu cha Issa Nasser Ismaily: ‘’Zanzibar: Kinyang’anyiro na Utumwa,’’ (1999). Jumla ya vitabu hivi vilivyoandikwa na Wazanzibari wenyewe nilivyosoma ni tisa na inaelekeawale waliopinduliwa wameaandika vitabu vingi kupita waliofanya mapinduzi. Viko vitabu vingine kuhusu mapinduzi havikuandikwa na Wazanzibar lakini vinahusu Zanzibar na mapinduzi. Hivi nimevisoma lakini sikuvifanyia patio na kuna vitabu vilivyoandikwa na waliopindua nimevisoma lakini hapa sijavitaja.
Historia zilizoandikwa na waliopindua zinaeleza ubaya na uovu wa utawala wa Sultani. Historia zilizoandikwa na waliopinduliwa wao hueleza Zanzibar iliyokuwa imetulia na mahali pazuri pa kuishi. Waandishi hawa wanaieleza Zanzibar baada ya mapinduzi. Hii ni Zanzibar ya jela za mateso na mauaji, maisha ya shida, wasiwasi, vifungo na kesi zilizohukumiwa na Mahkama ya Wananchi. Katika vitabu hivi kwa wale waandishi waliobahatika kukimbia nchi wakiwa hai, wanaeleza maisha ya uhamishoni, faraja na ustawi katika nchi mpya walizohamia, iwe ni UAE, Oman au Ulaya. Katika vitabu hivi kuna mengi ambayo ingawa yakifahamika lakini hayakupata kuandikwa.
Kuna vitabu vilivyoandikwa na wale ambao sisi kwa miaka mingi tulikuwa tukiwaamini kuwa ndiyo wataalamu wa historia ya Zanzibar. Hawa ni waandishi kutoka Marekani na kwengineko duniani. Mfano wa Michael Lofchie: ‘’Zanzibar Background to Revolution,’’ (1965); Don Patterson, ‘’Revolution in Zanzibar: An American Cold War Tale,’’ (?); kwa kutaja vitabu vichache. Kitabu cha Lofchie inaaminika ndiyo kitabu cha kwanza kuandikwa kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Waandishi hawa wa kigeni wameandika historia ya Zanzibar kwa kuangalia yale ambayo wao wanaona yana umuhimu kwao kuelezwa na dunia ikayafahamu. Hivi ndivyo vitabu kwa miaka mingi vikiaminiwa na vikitegemewa kwingi kufundisha na kuieleza historia ya mapinduzi ya Zanzibar. Lakini ukweli ni kuwa vitabu hivi vimeacha mengi na ya muhimu katika kuielewa historia ya Zanzibar katika ukweli wake. Sababu kubwa ya upungufu huu ni kwa wao kuamini kuwa wao ndiyo wanayojua yote.
Katika historia ya mapinduzi wote wamenyanyua kalamu kueleza historia ya mapinduzi ya Zanzibar. Waliopindua wameandika halikadhalika waliopinduliwa. Ambao hawajaandika historia yao ni wale walinzi wa mapinduzi waliokuwa katika vyombo vya usalama na ulinzi wa mapinduzi. Hawa bado hawajapata ujasiri wa kueleza historia zao. Wako walioeleza waliyopitia katika kipindi kile lakini si kwa kuandika bali kwa kueleza waliyoshudia na hawa utawakuta katika kitabu cha Harith Ghassany: ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.’’ Hawa angalau wamejitokeza kueleza kwa majuto yale waliyofanya wakisema kuwa haikuwa kwa ridhaa yao bali walikuwa wakitii amri kutoka juu.
Utetezi huu haukuwanusuru wafuasi wa Hitler katika Mahakama ya Nuremberg kuhukumu kesi za wauaji na watesaji katika Vita Vya Pili Vya Dunia (1939 – 1945). Ahmed Rajab katika dibaji yake katika kitabu hiki kagusia kuwa ushahidi kama huu uliomo katika kitabu hiki cha Ibrahim Hussein unaweza kutumika katika mahakama kuwatia hatiani wale waliofanya vitendo viovu. Wako hadi le Wazanzibari ambao bado hawajaona haja ya kujuta kwa yale yaliyotokea katika mapinduzi. Wanadhani yale yaliyofanya yalistahili kufanywa na ilikuwa ikuwa wajibu kufanywa kuondoa kile waliochokiona dhulma. Wako Wazanzibari walioshiriki mapinduzi waliojitolea kabla ya kufa kwao kueleza maovu yote kama njia ya kuondoa joto walilokuwa wakibeba vifuani mwao kila wakikumbuka yaliyopita. Kwa wao kueleza yale ilikuwa tiba na pozo la nafsi zao. Ibrahim Hussein yeye kabeba jukumu la kueleza yote aliyoshuhudia na ndani ya kitabu hiki naamini hakubakisha kitu. Ingawa waliohusika na uovu ile wameingia kaburini midomo yao ikiwa wameifumba Ibrahim Hussein kayaweka wazi yote ili yabaki kama kumbukumbu kwetu sote.
Ibrahim Hussein kaeleza vifo alivyoshuhudia vya wafungwa vijana maarufu wa Kizanzibari kaweka majina yao na picha na kaeleza namna walivyouliwa. Nawaachia wasomaji wasome majina na kuangalia picha hizo ndani ya kitabu. Katika kumbukizi hizi zote kuna mengi ya kujifunza na hawa wanaotuandikia historia hii tuna deni kubwa kwao. Msomaji hata awe mjanja kiasi gani hatoweza kuikwepa athari ya kalamu ya Ibrahim Hussein katika ubongo wake awe anasoma sawasawa ya mistari au katikati ya mistari. Uandishi wa historia hii hauihitaji umahiri na kipaji cha mwandishi hata kidogo. Yale aliyopitia yanatosha kutoa kitabu kizuri, cha maana na mafunzo makubwa kwa jamii.
Historia ya Zanzibar baada ya mapinduzi ni historia nzito ambayo si rahisi mtu kuibeba kwa maana ya ukasimama mbele ya watu na ukaihadithia. Unaweza kwa wepesi kabisa ukahadithia yaliyotokea Auschwitz Poland Vita Vya Pili Vya Dunia jinsi Wayahudi walivyouawa. Haya mimi huyaeleza na nikapita bila ya moyo kusimama. Lakini siku zote ninapoihadithia historia ya Zanzibar huihadithia kwa tahadhari kubwa moyo wangu ukiwa mzito. Hii si katika yale yaliyotokea Kwa Bamkwe peke yake bali historia nzima hata hata baada ya mapinduzi na nyakati hizi tulizonazo za siasa ya vyama nyingi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Historia yote ya Zanzibar imegubikwa na damu na majonzi. Historia ambayo wino wake ni damu, jasho na vumbi si historia ambayo mwalimu ataisomesha darasani uso wake ukiwa na tabasamu. Waandishi wa historia hizi mfano wa Ibrahim Hussein ni watu wanaostahili kuheshimiwa sana kwa kutuhifadhiya yale ambayo pengine wengi tungependa kuyasahau.
Mwandishi wa kitabu hiki Ibrahim Hussein amekianza kitabu chake kwa kumfanya msomaji kwa muda ahame kutoka jina la kitabu ahamie kwenye rejea za vitabu kuhusu wafungwa maarufu duniani. Mwandishi anavipitia vitabu walivyoandika wafungwa hawa na wengine ambao si wafungwa bali ni waandishi wa riwaya lakini zinazohusu vifungo vya kutisha. Katika wafungwa hawa yumo Ngugi Wathiong’o ambae zamani akijulikana kama James Ngugi. Ibrahim Hussein kwa namna ya pekee kaingia katika orodha ya Wazanzibar walioandika historia ya mapinduzi na kutuwekea mengi ambayo kabla hayakufahamika. Ibrahim Hussein katika kitabu chake ameliondoa pazia kumwezesha msomaji kuwajua wale waliokuwa Kwa Bamkwe kwa kutaja majina yao na kuweka picha zao. Kwa ustadi mkubwa mwandishi anakuchukua katika safari ya kwenda Kwa Bamkwe. Anaanza kwa staili ya ‘’dramatis personae’’ kama William Shakespeare anavyowatambulisha wahusika katika michezo yake. Ibrahim Hussein anakupitisha msomaji na kukujulisha kwa wahusika wakuu ndani ya mnyororo wa mateso kwa kukuwekea picha na majina na kwa umahiri mkubwa anawatambulisha watu hawa (wengi wao wameshatangulia mbele ya haki) kwa msomaji.
Katika maelezo haya anatuchorea sura mbili za hawa watesaji wasio na huruma wala hisia za utu. Anaeleza sura yao wanayoonyesha mnapokutana marikiti na kutoleana salamu na sura ile ya chuma wanayovaa wanapokuwa kwenye shughuli zao za kuyalinda ‘’mapinduzi matukufu.’’ Kitabu hiki cha Ibrahim Hussein kinatia hofu na simanzi kubwa pale unapokutana na majina ya watu unaowafahamu na kusoma kuwa hawa walikuwa watesaji watu Kwa Bamkwe. Pamoja na majina ya watesaji na picha zao kuna majina na picha za waliokufa Kwa Bamkwe wakiwa katika mikono ya hawa watesaji. Mimi siwezi kuyataja majina hayo hapa nawaachia wasomaji wenyewe kuyasoma ndani ya kitabu. Katika hawa wapo wanaoingia katika historia ya Zanzibar kwa uzalendo wao na wametunukiwa Nishani ya Mapinduzi. Historia ya mapinduzi si nyepesi na waandishi wake ni watu walio na ushujaa wa aina yake. Halikadhalika ni muhimu wa kwa jamii kutambua kuwa wanafunzi wa historia hii na walimu wanaosomesha historia hii vyuoni wanakabiliana na uzito si rahisi kuueleza.
Kitabu hiki kinaongeza historia nyingine katika yale ambayo walipitia Wazanzibari waliofungwa katika kipindi kile kabla na baada ya mauaji ya Karume. Kitabu hiki kimeandikwa kwa staili ya kipekee ukifananisha na vitabu vilivyotangulia. Vitabu vilivyotangulia kutoka kalamu za wafungwa waliokuwa wanasiasa kuna wakati katika kusoma msomaji anapumzishwa kusoma mateso na unyama waliokuwa wakifanyiwa wafungwa hawa kwa sababu mwandishi ataeleza harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar. Hapa mwandishi ataeleza na yale ambayo yaliyotokea na sababu za kutokea na kwa sababu gani ilikuwa hivyo na mengineyo. Katika kitabu hiki Ibrahim Hussein kwa kuwa hakuwa mwanasiasa hukutani na historia za kura wala ugawaji wa majimbo kwa vyama vya siasa na wagombea wao katika uchaguzi. Hata hivyo Ibrahim Hussein hakuweza kuficha uzalendo wake na mapenzi yake kwa nchi yake kwani ndani ya kitabu kaweka picha na majina ya vijana wa Umma Party waliokusudia kuunda Jeshi la Ukombozi la Zanzibar baada ya mapinduzi. Hili halikuwa kwa sababu ya muungano.
Kitabu hiki kimehifadhi shajara, yaani ‘’diary,’’ ya yale yaliyokuwa yanatokea siku baada ya siku baada ya siku katika maisha kifungoni. Wakati mwingine unaweza kudhani kuwa hayo usomayo ni kutoka ukurasa wa kitabu maarufu ‘’Papillon,’’ kilichoandikwa na Henri Charriere kitabu kinachoeleza shida na mateso katika jela iliyokuwa katika kisiwa kilichopewa jina la kutisha, ‘’Devil’s Island’’ yaani ‘’Kisiwa cha Shetani.’’ Halikadhalika wakati mwingine unaweza kusema labda unasoma ukurasa kutoka yale ya kutisha ndani ya jela maarufu ya Alcatraz. Lakini kila kidole chako kinapofungua ukurasa mwandishi anakukumbusha kuwa hauko Alcatraz wala Devil’s Island bali uko Zanzibar, Kwa Bamkwe. Jela hizi mbili zote leo hazipo zimefungwa na sasa ni sehemu ya historia katika makumbusho. Yawezekana siku moja Kiinua Miguu nayo ikawa sehemu ya historia ya Zanzibar. Wazanzibari watapenda kuisahau Kwa Bamkwe na yote yaliyofanyika pale. Kwa Bamkwe na watendaji wake watasomwa kama historia mbaya iliyopita mfano wa Wajerumani wanavyoisoma historia ya Hitler na Gestapo.
Kitabu hiki naamini kitawagusa Wazanzibari wengi wa kizazi kilichoshuhudia mapinduzi kwa namna nyingi kuanzia kuyasoma yale yaliyokuwako kabla na baada ya mapinduzi na pia na hili ndilo muhimu zaidi kufahamu ukweli wa historia yote hadi kupelekea mauaji ya Abeid Amani Karume. Wengi katika hawa wametangulia mbele ya haki na wengine bado wapo na pengine wapo hapa ukumbini. Katika hawa waliokamatwa na kuwekwa kizuizini na kuteswa wako wengine walikuja baadae kuwa viongozi wa juu Zanzibar na wakatoa mchango mkubwa katika kuvitafutia visiwa hivi amani na maendeleo.
Mohamed Said​
16 August 2024